119.1 Tusome kwanza maandiko katika Zaburi 119:1-176
Back to: KOZI 119: KITABU CHA ZABURI
ZABURI 119:1-176
- Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.
- Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.
- Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake.
- Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana.
- Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako.
- Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote.
- Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako
- Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa
- Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
- Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
- Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
- Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.
- Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako.
- Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi.
- Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako.
- Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.
- Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
- Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
- Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.
- Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati.
- Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
- Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
- Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
- Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu.
- Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.
- Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.
- Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako.
- Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
- Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako.
- Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
- Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe.
- Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu.
- Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho.
- Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
- Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo.
- Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa.
- Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.
- Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako.
- Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema.
- Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako.
- Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
- Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako.
- Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako.
- Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele.
- Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
- Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu.
- Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.
- Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.
- Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha.
- Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.
- Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako.
- Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji.
- Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako.
- Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu.
- Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako.
- Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
- Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.
- Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.
- Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.
- Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.
- Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.
- Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.
- Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.
- Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.
- Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.
- Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.
- Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako.
- Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako.
- Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.
- Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako.
- Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.
- Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
- Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.
- Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako.
- Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
- Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
- Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.
- Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako.
- Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako.
- Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.
- Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako.
- Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji?
- Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako.
- Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?
- Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.
- Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie.
- Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako.
- Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
- Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele.
- Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.
- Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.
- Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu.
- Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha.
- Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako.
- Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako.
- Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno.
- Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
- Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote.
- Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
- Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.
- Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako.
- Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.
- Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.
- Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
- Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
- Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.
- Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.
- Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.
- Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.
- Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.
- Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.
- Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.
- Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda.
- Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea.
- Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
- Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
- Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima.
- Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo.
- Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
- Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako.
- Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
- Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee.
- Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako.
- Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.
- Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako.
- Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
- Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
- Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.
- Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.
- Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.
- Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako.
- Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.
- Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki.
- Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako.
- Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.
- Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako.
- Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.
- Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.
- Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.
- Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.
- Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako.
- Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.
- Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu.
- Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi.
- Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako.
- Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako.
- Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.
- Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako.
- Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako.
- Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako.
- Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli.
- Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele.
- Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.
- Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.
- Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.
- Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.
- Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.
- Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.
- Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.
- Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
- Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.
- Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi.
- Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda.
- Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.
- Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.
- Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda.
- Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno.
- Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.
- Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako.
- Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako.
- Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.
- Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki.
- Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako.
- Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.
- Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie.
- Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.
YESU.PROSHABO.COM
0