4.1 Tusome kwanza maandiko katika Mwanzo 4.1-26
Back to: MWANZO
MWANZO 4:1-26
- Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.
- Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
- Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana.
- Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;
- bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
- Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
- Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
- Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.
- Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?
- Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.
- Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;
- utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.
- Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.
- Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.
- Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.
- Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.
- Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.
- Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki.
- Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.
- Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.
- Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.
- Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.
- Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;
- Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
- Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
- Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.
YESU.PROSHABO.COM
0